| Chapter 20 |
1 | "Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake.
|
2 | Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu.
|
3 | Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi.
|
4 | Akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.`
|
5 | Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo.
|
6 | Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, `Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?`
|
7 | Wakamjibu: `Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.` Yeye akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.`
|
8 | "Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, `Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.`
|
9 | Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja dinari moja.
|
10 | Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.
|
11 | Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung`unikia yule bwana.
|
12 | Wakasema, `Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?`
|
13 | "Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, `Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja?
|
14 | Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.
|
15 | Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?"`
|
16 | Yesu akamaliza kwa kusema, "Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho."
|
17 | Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,
|
18 | "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe.
|
19 | Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa."
|
20 | Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.
|
21 | Yesu akamwuliza, "Unataka nini?" Huyo mama akamwambia, "Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto."
|
22 | Yesu akajibu, "Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?" Wakamjibu, "Tunaweza."
|
23 | Yesu akawaambia, "Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu."
|
24 | Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili.
|
25 | Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu wao.
|
26 | Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;
|
27 | na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu.
|
28 | Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi."
|
29 | Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata.
|
30 | Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!"
|
31 | Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!"
|
32 | Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, "Mnataka niwafanyie nini?"
|
33 | Wakamjibu, "Mheshimiwa, tunaomba macho yetu yafumbuliwe."
|
34 | Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.
|