| Chapter 25 |
1 | "Wakati huo, Ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi.
|
2 | Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.
|
3 | Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta.
|
4 | Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao.
|
5 | Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wanawali wote wote walisinzia, wakalala.
|
6 | Usiku wa manane kukawa na kelele: `Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.`
|
7 | Hapo wale wanawali wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao.
|
8 | Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: `Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.`
|
9 | Lakini wale wenye busara wakawaambia, `Hayatatutosha sisi na ninyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!`
|
10 | Basi, wale wanawali wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la arusi, kisha mlango ukafungwa.
|
11 | Baadaye wale wanawali wengine wakaja, wakaita: `Bwana, bwana, tufungulie!`
|
12 | Lakini yeye akawajibu, `Nawaambieni kweli, siwajui ninyi."`
|
13 | Kisha Yesu akasema, "Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.
|
14 | "Itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ng`ambo: aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake.
|
15 | Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: mmoja sarafu tano za fedha ziitwazo talanta, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.
|
16 | Mara yule aliyekabidhiwa talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.
|
17 | Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.
|
18 | Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaenda akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake.
|
19 | "Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake.
|
20 | Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano akaja amechukua zile talanta tano faida, akamwambia, `Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.`
|
21 | Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`
|
22 | "Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, `Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.`
|
23 | Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`
|
24 | "Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, `Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya.
|
25 | Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.`
|
26 | "Bwana wake akamwambia, `Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya.
|
27 | Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake!
|
28 | Basi, mnyang`anyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi.
|
29 | Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
|
30 | Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.`
|
31 | "Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu,
|
32 | na mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi.
|
33 | Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.
|
34 | "Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, `Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni Ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
|
35 | Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha;
|
36 | nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.`
|
37 | Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme `Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji?
|
38 | Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika?
|
39 | Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?`
|
40 | Mfalme atawajibu, `Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.`
|
41 | "Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, `Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake.
|
42 | Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji.
|
43 | Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.`
|
44 | "Hapo nao watajibu, `Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukuja kukuhudumia?`
|
45 | Naye atawajibu, `Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.`
|
46 | Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uzima wa milele."
|