| Chapter 4 |
1 | Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa.
|
2 | Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia,
|
3 | "Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.
|
4 | Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila.
|
5 | Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Mbegu hizo ziliota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina.
|
6 | Jua lilipochomoza, zikachomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka.
|
7 | Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka.
|
8 | Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikakua na kuzaa: moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia."
|
9 | Kisha akawaambia, "Mwenye masikio na asikie!"
|
10 | Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano.
|
11 | Naye akawaambia, "Ninyi mmejaliwa kujua siri ya Utawala wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano,
|
12 | ili, `Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe."`
|
13 | Basi, Yesu akawauliza, "Je, ninyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote?
|
14 | Mpanzi hupanda neno la Mungu.
|
15 | Watu wengine ni kama wale walio njiani ambapo mbegu zilianguka. Hawa hulisikia hilo neno lakini mara Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao.
|
16 | Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu wanapolisikia hilo neno hulipokea kwa furaha.
|
17 | Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno mara wanakata tamaa.
|
18 | Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaolisikia hilo neno,
|
19 | lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda.
|
20 | Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia moja."
|
21 | Yesu akaendelea kuwaambia, "Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa pishi au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara.
|
22 | Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa.
|
23 | Mwenye masikio na asikie!"
|
24 | Akawaambia pia, "Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa.
|
25 | Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa."
|
26 | Yesu akaendelea kusema, "Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani.
|
27 | Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika.
|
28 | Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke.
|
29 | Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika."
|
30 | Tena, Yesu akasema, "Tuufananishe Utawala wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani?
|
31 | Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote.
|
32 | Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake."
|
33 | Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia.
|
34 | Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.
|
35 | Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Tuvuke ziwa, twende ng`ambo."
|
36 | Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Palikuwapo pia mashua nyingine hapo.
|
37 | Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji.
|
38 | Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, "Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?"
|
39 | Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, "Kimya! Tulia!" Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa.
|
40 | Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?"
|
41 | Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, "Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?"
|