| Chapter 13 |
1 | Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!"
|
2 | Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa."
|
3 | Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha,
|
4 | "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?"
|
5 | Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
|
6 | Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, `Mimi ndiye!` nao watawapotosha watu wengi.
|
7 | Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
|
8 | Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto.
|
9 | "Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao.
|
10 | Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote.
|
11 | Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu.
|
12 | Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.
|
13 | Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.
|
14 | "Mtakapoona `Chukizo Haribifu` limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani.
|
15 | Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu.
|
16 | Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
|
17 | Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!
|
18 | Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi.
|
19 | Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena.
|
20 | Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo.
|
21 | "Basi mtu akiwaambieni, `Tazama, Kristo yupo hapa!` au `Yupo pale!` msimsadiki.
|
22 | Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana.
|
23 | Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.
|
24 | "Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza.
|
25 | Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.
|
26 | Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu.
|
27 | Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
|
28 | "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
|
29 | Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana.
|
30 | Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.
|
31 | Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
|
32 | "Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.
|
33 | Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini.
|
34 | Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho.
|
35 | Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi.
|
36 | Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.
|
37 | Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"
|