| Chapter 1 |
1 | Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu.
|
2 | Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo.
|
3 | Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango,
|
4 | ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.
|
5 | Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni.
|
6 | Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama.
|
7 | Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.
|
8 | Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,
|
9 | Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani.
|
10 | Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.
|
11 | Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani.
|
12 | Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
|
13 | Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.
|
14 | Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
|
15 | Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.
|
16 | Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.
|
17 | Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake."
|
18 | Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu."
|
19 | Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema.
|
20 | Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia."
|
21 | Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni.
|
22 | Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
|
23 | Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.
|
24 | Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema:
|
25 | "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu."
|
26 | Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya,
|
27 | kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi.
|
28 | Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe."
|
29 | Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini?
|
30 | Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.
|
31 | Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu.
|
32 | Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake.
|
33 | Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho."
|
34 | Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?"
|
35 | Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu.
|
36 | Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.
|
37 | Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu."
|
38 | Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.
|
39 | Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda.
|
40 | Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti.
|
41 | Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu,
|
42 | akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa.
|
43 | Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
|
44 | Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
|
45 | Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia."
|
46 | Naye Maria akasema,
|
47 | "Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
|
48 | Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
|
49 | Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.
|
50 | Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.
|
51 | Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
|
52 | amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.
|
53 | Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
|
54 | Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.
|
55 | Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele."
|
56 | Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
|
57 | Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.
|
58 | Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
|
59 | Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya.
|
60 | Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane."
|
61 | Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?"
|
62 | Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.
|
63 | Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu.
|
64 | Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
|
65 | Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea.
|
66 | Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
|
67 | Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu:
|
68 | "Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake.
|
69 | Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake.
|
70 | Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu,
|
71 | kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
|
72 | Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu.
|
73 | Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi
|
74 | tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu,
|
75 | kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu.
|
76 | Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;
|
77 | kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao.
|
78 | Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu,
|
79 | na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani."
|
80 | Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.
|