| Chapter 12 |
1 | Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, "Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki.
|
2 | Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa.
|
3 | Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonong`ona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba.
|
4 | "Nawaambieni ninyi rafiki zangu: msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi.
|
5 | Nitawaonyesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo.
|
6 | Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja.
|
7 | Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi, ninyi mna thamani zaidi kuliko shomoro wengi!
|
8 | "Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake.
|
9 | Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.
|
10 | "Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.
|
11 | "Watakapowapeleka ninyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema.
|
12 | Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema."
|
13 | Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, "Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba."
|
14 | Yesu akamjibu, "Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi mwamuzi au msuluhishi kati yenu?"
|
15 | Basi, akawaambia wote, "Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo."
|
16 | Kisha akawaambia mfano: "Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi.
|
17 | Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: `Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu?
|
18 | Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, na humo nitahifadhi mavuno yangu yote na mali yangu.
|
19 | Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, ule, unywe na kufurahi.`
|
20 | Lakini Mungu akamwambia: `Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojilundikia vitakuwa vya nani?"`
|
21 | Yesu akamaliza kwa kusema "Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejilundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu."
|
22 | Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu.
|
23 | Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi.
|
24 | Chukueni kwa mfano, kunguru: hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Ninyi mna thamani zaidi kuliko ndege!
|
25 | Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi anaweza kuongeza urefu wa maisha yake?
|
26 | Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine?
|
27 | Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Hata hivyo, nawahakikishieni kwamba hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.
|
28 | Lakini, kama Mungu hulivika vizuri jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatawafanyia ninyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!
|
29 | "Basi, msivurugike akili, mkihangaika daima juu ya mtakachokula au mtakachokunywa.
|
30 | Kwa maana hayo yote ndiyo yanayohangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo.
|
31 | Shughulikieni kwanza Ufalme wa Mungu, na hayo yote mtapewa kwa ziada.
|
32 | "Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni Ufalme.
|
33 | Uzeni mali yenu mkawape maskini misaada. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na jiwekeeni hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu.
|
34 | Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
|
35 | "Muwe tayari! Jifungeni mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka;
|
36 | muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka arusini, ili wamfungulie mara atakapobisha hodi.
|
37 | Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia.
|
38 | Heri yao watumishi hao ikiwa bwana wao atawakuta wanakesha hata ikiwa atarudi usiku wa manane au alfajiri.
|
39 | Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
|
40 | Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."
|
41 | Petro akamwambia, "Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?"
|
42 | Bwana akajibu, "Ni nani basi, mtumishi aliye mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao?
|
43 | Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.
|
44 | Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote.
|
45 | Lakini, kama mtumishi huyo atafikiri moyoni mwake: na kusema: `Bwana wangu amekawia sana kurudi` halafu aanze kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa,
|
46 | bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamkatilia mbali na kumweka fungu moja na wasioamini.*fb*
|
47 | Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana.
|
48 | Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atatakiwa vingi; aliyekabidhiwa vingi zaidi atatakiwa kutoa vingi zaidi.
|
49 | "Nimekuja kuwasha moto duniani, laiti ungekuwa umewaka tayari!
|
50 | Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike!
|
51 | Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano.
|
52 | Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu.
|
53 | Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mama mkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mama mkwe wake."
|
54 | Yesu akayaambia tena makundi ya watu, "Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: `Mvua itanyesha`, na kweli hunyesha.
|
55 | Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema `Kutakuwa na hali ya joto` na ndivyo inavyokuwa.
|
56 | Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia dunia na anga; kwa nini basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi?
|
57 | "Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya?
|
58 | Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani.
|
59 | Hakika hutatoka huko nakwambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho."
|