| Chapter 15 |
1 | Siku moja, watoza ushuru na wahalifu wengi walikwenda kumsikiliza Yesu.
|
2 | Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kunung`unika: "Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao."
|
3 | Yesu akawajibu kwa mfano:
|
4 | "Hivi, mtu akiwa na kondoo mia, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate.
|
5 | Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha.
|
6 | Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake akiwaambia, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.`
|
7 | Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu. ic
|
8 | "Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, aifagie nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate.
|
9 | Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake akisema, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.`
|
10 | Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu."
|
11 | Yesu akaendelea kusema, "Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili.
|
12 | Yule mdogo, alimwambia baba yake: `Baba, nipe urithi wangu.` Naye akawagawia mali yake.
|
13 | Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo.
|
14 | Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika.
|
15 | Akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe.
|
16 | Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu.
|
17 | Alipoanza kupata akili akafikiri: `Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa?
|
18 | Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia.
|
19 | Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.`
|
20 | Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu.
|
21 | "Mwanawe akamwambia: `Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.`
|
22 | Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: `Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu!
|
23 | Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea!
|
24 | Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.` Wakaanza kufanya sherehe.
|
25 | "Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani akasikia vifijo na ngoma.
|
26 | Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: `Kuna nini?`
|
27 | Huyo mtumishi akamwambia: `Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.`
|
28 | Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie.
|
29 | Lakini yeye akamjibu: `Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwana mbuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu!
|
30 | Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.`
|
31 | Baba yake akamjibu: `Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako.
|
32 | Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana."`
|