| Chapter 19 |
1 | Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za mji huo.
|
2 | Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri.
|
3 | Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu.
|
4 | Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo.
|
5 | Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako."
|
6 | Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha.
|
7 | Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung`unika wakisema, "Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi."
|
8 | Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang`anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne."
|
9 | Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu.
|
10 | Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea." ic
|
11 | Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. (Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, Ufalme wa Mungu ungefika.)
|
12 | Hivyo akawaambia, "Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi.
|
13 | Basi, kabla ya kuondoka aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kumwambia: `Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.`
|
14 | Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: `Hatumtaki huyu atutawale.`
|
15 | "Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani.
|
16 | Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.`
|
17 | Naye akamwambia: `Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!`
|
18 | Mtumishi wa pili akaja, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.`
|
19 | Naye akamwambia pia: `Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.`
|
20 | "Mtumishi mwingine akaja, akasema: `Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa,
|
21 | kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na huchuma ambacho hukupanda.`
|
22 | Naye akamwambia: `Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda.
|
23 | Kwa nini basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?`
|
24 | Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: `Mnyang`anyeni hizo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.`
|
25 | Nao wakamwambia: `Lakini Mheshimiwa, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!`
|
26 | Naye akawajibu: `Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
|
27 | Na sasa, kuhusu hao maadui wangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu."`
|
28 | Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu.
|
29 | Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,
|
30 | akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa.
|
31 | Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni, `Bwana ana haja naye."`
|
32 | Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia.
|
33 | Walipokuwa wanamfungua yule mwana punda, wenyewe wakawauliza, "Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?"
|
34 | Nao wakawajibu, "Bwana anamhitaji."
|
35 | Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu.
|
36 | Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani.
|
37 | Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona;
|
38 | wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!"
|
39 | Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!"
|
40 | Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti."
|
41 | Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia
|
42 | akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako.
|
43 | Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote.
|
44 | Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa."
|
45 | Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje wafanyabiashara
|
46 | akisema, "Imeandikwa: `Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala`; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi."
|
47 | Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza,
|
48 | lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.
|