| Chapter 22 |
1 | Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia.
|
2 | Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu.
|
3 | Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwae Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili.
|
4 | Yuda akaenda akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa Hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao.
|
5 | Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha.
|
6 | Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua.
|
7 | Basi, siku ya Mikate Isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa.
|
8 | Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, "Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka."
|
9 | Nao wakamwuliza, "Unataka tuiandae wapi?"
|
10 | Akawaambia, "Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia.
|
11 | Mwambieni mwenye nyumba: `Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?`
|
12 | Naye atawaonyesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo."
|
13 | Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka.
|
14 | Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake.
|
15 | Akawaambia, "Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu.
|
16 | Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika Ufalme wa Mungu."
|
17 | Kisha akatwaa kikombe, akashukuru akasema, "Pokeeni, mgawanye ninyi kwa ninyi.
|
18 | Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja."
|
19 | Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, "Huu ni mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka."
|
20 | Akafanya vivyo hivyo na kikombe, baada ya chakula, akisema, "Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu.*fd*
|
21 | "Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani.
|
22 | Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti."
|
23 | Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo.
|
24 | Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu zaidi kuliko wengine.
|
25 | Yesu akawaambia, "Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu.
|
26 | Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi.
|
27 | Kwa maana, ni nani aliye mkuu: yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi.
|
28 | "Ninyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu;
|
29 | na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi Ufalme, vivyo hivyo nami nitawakabidhi ninyi Ufalme.
|
30 | Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na mtaketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
|
31 | "Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta ninyi kama mtu anavyopepeta ngano.
|
32 | Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako."
|
33 | Naye Petro akamjibu, "Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa."
|
34 | Yesu akamjibu, "Nakwambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu."
|
35 | Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, "Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?" Wakajibu, "La."
|
36 | Naye akawaambia, "Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja.
|
37 | Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: `Aliwekwa kundi moja na wahalifu,` ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake."
|
38 | Nao wakasema, "Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili." Naye akasema, "Basi!"
|
39 | Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata.
|
40 | Alipofika huko akawaambia, "Salini, msije mkaingia katika kishawishi."
|
41 | Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali:
|
42 | "Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu."
|
43 | Hapo, malaika kutoka mbinguni, akamtokea ili kumtia moyo.
|
44 | Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka, kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini.*fe* ic
|
45 | Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni.
|
46 | Akawaambia, "Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi."
|
47 | Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu.
|
48 | Lakini Yesu akamwambia, "Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?"
|
49 | Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, "Bwana, tutumie panga zetu?"
|
50 | Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio lake la kulia.
|
51 | Hapo, Yesu akasema, "Acha! Hii inatosha." Akaligusa sikio la mtu huyo akaliponya.
|
52 | Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuja kumkamata: "Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang`anyi?
|
53 | Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku Hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza."
|
54 | Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali.
|
55 | Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa miongoni mwao.
|
56 | Mjakazi mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, "Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu."
|
57 | Lakini Petro akakana akisema, "Wee! simjui mimi."
|
58 | Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, "Wewe ni mmoja wao." Lakini Petro akajibu "Bwana we; si mimi!"
|
59 | Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, "Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati."
|
60 | Lakini Petro akasema, "Bwana wee; sijui hata unachosema!" Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika.
|
61 | Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: "Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu."
|
62 | Hapo akatoka nje, akalia sana.
|
63 | Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki.
|
64 | Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, "Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!"
|
65 | Wakamtolea maneno mengi ya matusi.
|
66 | Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika, ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Yesu akaletwa mbele ya Baraza hilo.
|
67 | Nao wakamwambia, "Twambie! Je, wewe ndiwe Kristo?" Lakini Yesu akawaambia, "Hata kama nikiwaambieni, hamtasadiki;
|
68 | na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu.
|
69 | Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenyezi."
|
70 | Hapo wote wakasema, "Ndiyo kusema wewe ni Mwana wa Mungu?" Naye akasema, "Ninyi mnasema kwamba mimi ndiye."
|
71 | Nao wakasema, "Je, tunahitaji ushahidi mwingine? Sisi wenyewe tumesikia akisema kwa mdomo wake mwenyewe."sw4323
|