| Chapter 24 |
1 | Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha.
|
2 | Walikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi.
|
3 | Walipoingia ndani, hawakuona mwili wa Bwana Yesu.
|
4 | Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kung`aa sana, wakasimama karibu nao.
|
5 | Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, "Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu?
|
6 | Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya:
|
7 | `Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha, na siku ya tatu atafufuka."`
|
8 | Hapo wanawake wakayakumbuka maneno yake,
|
9 | wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wengine habari za mambo hayo yote.
|
10 | Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao.
|
11 | Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini.
|
12 | Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.
|
13 | Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu.
|
14 | Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia.
|
15 | Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao.
|
16 | Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua.
|
17 | Akawauliza, "Mnazungumza nini huku mnatembea?" Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni.
|
18 | Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, "Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?"
|
19 | Naye akawajibu, "Mambo gani?" Wao wakamjibu, "Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote.
|
20 | Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha.
|
21 | Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka.
|
22 | Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi,
|
23 | wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai.
|
24 | Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona."
|
25 | Kisha Yesu akawaambia, "Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii?
|
26 | Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?"
|
27 | Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote.
|
28 | Walipokikaribia kile kijiji walikokuwa wanakwenda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari;
|
29 | lakini wao wakamsihi wakisema, "Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia." Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao.
|
30 | Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
|
31 | Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao.
|
32 | Basi, wakaambiana, "Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?"
|
33 | Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika
|
34 | wakisema, "Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni."
|
35 | Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.
|
36 | Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia "Amani kwenu."
|
37 | Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu.
|
38 | Lakini yeye akawaambia, "Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu?
|
39 | Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkanione, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo."
|
40 | Baada ya kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu.
|
41 | Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, "Mnacho chakula chochote hapa?"
|
42 | Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.
|
43 | Akakichukua, akala, wote wakimwona.
|
44 | Halafu akawaambia, "Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika Sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi."
|
45 | Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu.
|
46 | Akawaambia, "Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka wafu,
|
47 | na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia na Yerusalemu yahubiriwe juu ya kutubu na kusamehewa dhambi.
|
48 | Ninyi ni mashahidi wa mambo hayo.
|
49 | Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu."
|
50 | Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki.
|
51 | Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni.
|
52 | Wao wakamwabudu, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa:
|
53 | wakakaa muda wote Hekaluni wakimsifu Mungu.
|