| Chapter 3 |
1 | Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake Nikodemo.
|
2 | Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye."
|
3 | Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu."
|
4 | Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!"
|
5 | Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.
|
6 | Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho.
|
7 | Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya.
|
8 | Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho."
|
9 | Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya yanawezekanaje?"
|
10 | Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel na huyajui mambo haya?
|
11 | Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini ninyi hamkubali ujumbe wetu.
|
12 | Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni?
|
13 | Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu ambaye ameshuka kutoka mbinguni.
|
14 | "Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo,
|
15 | ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele.
|
16 | Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
|
17 | Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe ulimwengu.
|
18 | "Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu.
|
19 | Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu.
|
20 | Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe.
|
21 | Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu."
|
22 | Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu.
|
23 | Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza.
|
24 | Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.)
|
25 | Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha.
|
26 | Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, "Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng`ambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea."
|
27 | Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu.
|
28 | Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: `Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!`
|
29 | Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa.
|
30 | Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue.
|
31 | "Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wote.
|
32 | Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe wake.
|
33 | Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli.
|
34 | Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo.
|
35 | Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote.
|
36 | Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana hatakuwa na uzima wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake."
|