| Chapter 13 |
1 | Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho!
|
2 | Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu.
|
3 | Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu.
|
4 | Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni.
|
5 | Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia.
|
6 | Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, "Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?"
|
7 | Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye."
|
8 | Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena."
|
9 | Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia."
|
10 | Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Ninyi mmetakata, lakini si nyote."
|
11 | Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: "Ninyi mmetakata, lakini si nyote.")
|
12 | Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?
|
13 | Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi.
|
14 | Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu.
|
15 | Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni.
|
16 | Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma.
|
17 | Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
|
18 | "Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: `Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.`
|
19 | Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa mimi ndimi.
|
20 | Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma."
|
21 | Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!"
|
22 | Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani.
|
23 | Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.
|
24 | Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: "Mwulize anasema juu ya nani."
|
25 | Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, "Bwana, ni nani?"
|
26 | Yesu akajibu, "Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye." Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.
|
27 | Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, "Unachotaka kufanya, kifanye haraka!"
|
28 | Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.
|
29 | Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa fedha, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini.
|
30 | Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.
|
31 | Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, "Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
|
32 | Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara.
|
33 | "Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu. Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: `Niendako ninyi hamwezi kwenda!`
|
34 | Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.
|
35 | Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu."
|
36 | Simoni Petro akamwuliza, "Bwana, unakwenda wapi?" Yesu akajibu, "Niendako huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye."
|
37 | Petro akamwambia "Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Niko tayari kufa kwa ajili yako!"
|
38 | Yesu akajibu, "Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili yangu? Kweli nakwambia, kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!"
|