| Chapter 10 |
1 | Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima.
|
2 | Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli.
|
3 | Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu.
|
4 | Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu.
|
5 | Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi."
|
6 | Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: `Nani atapanda mpaka mbinguni?` (yaani, kumleta Kristo chini);
|
7 | wala usiseme: `Nani atashuka mpaka Kuzimu` (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu)."
|
8 | Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile imani tunayoihubiri.
|
9 | Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka.
|
10 | Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu; na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa.
|
11 | Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye hatakuwa na sababu ya kuaibika."
|
12 | Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao.
|
13 | Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa."
|
14 | Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri?
|
15 | Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!"
|
16 | Lakini wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?"
|
17 | Hivyo basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo.
|
18 | Lakini nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu."
|
19 | Tena nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu."
|
20 | Tena Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu."
|
21 | Lakini kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii."
|