| Chapter 3 |
1 | Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo.
|
2 | Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari.
|
3 | Maana bado mu watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na magombano kati yenu? Mambo hayo yanaonyesha wazi kwamba ninyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia.
|
4 | Mmoja wenu anaposema, "Mimi ni wa Paulo", na mwingine, "Mimi ni wa Apolo", je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu?
|
5 | Apolo ni nani? na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu ambao tuliwaleteeni ninyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na Bwana.
|
6 | Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini aliyeiotesha mbegu ni Mungu.
|
7 | Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota.
|
8 | Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa, ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe.
|
9 | Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na ninyi ni shamba lake; ninyi ni jengo lake.
|
10 | Kwa msaada wa neema aliyonipa Mungu, nimefaulu, kama mwashi stadi mwenye busara, kuweka msingi ambao juu yake mtu mwingine anajenga. Basi, kila mmoja awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake.
|
11 | Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo.
|
12 | Juu ya msingi huo mtu anaweza kujenga kwa dhahabu, fedha au mawe ya thamani; anaweza kutumia miti, majani au nyasi.
|
13 | Iwe iwavyo, ubora wa kazi ya kila mmoja utaonekana wakati Siku ile ya Kristo itakapoifichua. Maana, Siku hiyo itatokea na moto, na huo moto utaipima na kuonyesha ubora wake.
|
14 | Ikiwa alichojenga mtu juu ya huo msingi kitaustahimili huo moto, atapokea tuzo;
|
15 | lakini kama alichojenga kitaunguzwa, basi, atapoteza tuzo lake; lakini yeye mwenyewe ataokolewa kana kwamba ameponyoka kutoka motoni.
|
16 | Je, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
|
17 | Basi, mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu; maana hekalu la Mungu ni takatifu, na hekalu hilo ni ninyi wenyewe.
|
18 | Msijidanganye! Mtu yeyote miongoni mwenu akijidhania mwenye hekima mtindo wa kidunia, heri awe mjinga kusudi apate kuwa na hekima ya kweli.
|
19 | Maana, hekima ya kidunia ni upumbavu mbele ya Mungu. Kwani Maandiko Matakatifu yasema: "Mungu huwanasa wenye hekima katika ujanja wao."
|
20 | Na tena: "Bwana ajua kwamba mawazo ya wenye hekima hayafai."
|
21 | Basi, mtu asijivunie watu. Maana kila kitu ni chenu.
|
22 | Paulo, Apolo na Kefa, ulimwengu, maisha na kifo; mambo ya sasa na ya baadaye, yote ni yenu.
|
23 | Lakini ninyi ni wa Kristo naye Kristo ni wa Mungu.
|