| Chapter 11 |
1 | Niigeni mimi kama ninavyomwiga Kristo.
|
2 | Nawapeni hongera kwa sababu mnanikumbuka na kwa sababu mnayashikilia yale maagizo niliyowapeni.
|
3 | Lakini napenda pia mjue kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, na mwanamume ni kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo.
|
4 | Basi, kila mwanamume anayesali au anayetangaza ujumbe wa Mungu huku amefunika kichwa chake, huyo anamdharau Kristo.
|
5 | Na mwanamke akisali au kutangaza ujumbe wa Mungu bila kufunika kichwa chake, anamdharau mumewe; anayefanya hivyo ni sawa tu na mwanamke aliyenyoa kichwa chake.
|
6 | Mwanamke asiyefunika kichwa chake, afadhali anyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa; basi, afadhali afunike kichwa chake.
|
7 | Haifai mwanamume kufunika kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na kioo cha utukufu wake Mungu; lakini mwanamke ni kioo cha utukufu wa mwanamume.
|
8 | Mwanamume hakutoka kwa mwanamke, ila mwanamke alitoka kwa mwanamume.
|
9 | Mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, ila mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanamume.
|
10 | Ndiyo maana mwanamke hufunika kichwa chake, iwe ishara ya mamlaka yaliyo juu yake, na pia kwa sababu ya malaika.
|
11 | Hata hivyo, mbele ya Bwana mwanamke si kitu bila mwanamume, naye mwanamume si kitu bila mwanamke.
|
12 | Kama vile mwanamke alivyotokana na mwanamume, vivyo hivyo mwanamume huzaliwa na mwanamke; kila kitu hutoka kwa Mungu.
|
13 | Amueni wenyewe: Je, inafaa mwanamke kumwomba Mungu bila kuvaa kitu kichwani?
|
14 | Hata maumbile yenyewe huonyesha wazi kwamba kwa mwanamume kuwa na nywele ndefu ni aibu kwake mwenyewe;
|
15 | lakini kwa mwanamke kuwa na nywele ni heshima kwake; nywele zake ndefu amepewa ili zimfunike.
|
16 | Kama mtu anataka kuleta ubishi juu ya jambo hili, basi, na ajue kwamba sisi hatuna desturi nyingine, wala makanisa ya Mungu hayana desturi nyingine.
|
17 | Nikiwa bado nawapeni maagizo haya, siwezi hata kidogo kuwapa ninyi hongera kuhusu haya yafuatayo: mikutano yenu ninyi waumini yaleta hasara zaidi kuliko faida.
|
18 | Awali ya yote, nasikia kwamba mnapokutana pamoja hutokea mafarakano kati yenu. Nami naamini kiasi,
|
19 | maana ni lazima fikira tofauti ziweko miongoni mwenu, ili wale walio thabiti wapate kutambulikana.
|
20 | Kweli mnakutana, lakini si kwa ajili ya kula chakula cha Bwana!
|
21 | Maana mnapokula kila mmoja hukikalia chakula chake mwenyewe, hata hutokea kwamba baadhi yenu wana njaa, na wengine wamelewa!
|
22 | Je, hamwezi kula na kunywa nyumbani kwenu! Au je, mnalidharau kanisa la Mungu na kuwaaibisha hao wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? La hasha! Si kuhusu jambo hili.
|
23 | Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: kwamba, usiku ule Bwana Yesu aliotolewa, alitwaa mkate,
|
24 | akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: "Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka."
|
25 | Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe akasema: "Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka."
|
26 | Maana kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja.
|
27 | Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana.
|
28 | Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho;
|
29 | maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe.
|
30 | Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa.
|
31 | Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo.
|
32 | Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
|
33 | Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutana kula chakula cha Bwana, kila mmoja amngoje mwenzake.
|
34 | Na kama kuna yeyote aliye na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutana kwenu kusisababishe hukumu. Lakini, kuhusu yale mambo mengine, nitawapeni maelezo nitakapokuja.
|