| Chapter 6 |
1 | Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa.
|
2 | Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.
|
3 | Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe.
|
4 | Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine.
|
5 | Maana kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba.
|
6 | Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.
|
7 | Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna.
|
8 | Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.
|
9 | Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake.
|
10 | Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.
|
11 | Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe.
|
12 | Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.
|
13 | Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki Sheria; huwataka ninyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu.
|
14 | Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.
|
15 | Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya.
|
16 | Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli--Wateule wa Mungu.
|
17 | Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu.
|
18 | Ndugu, nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Kristo. Amina.
|