| Chapter 2 |
1 | Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena.
|
2 | Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa.
|
3 | Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mmegundua kwamba Bwana ni mwema."
|
4 | Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule, na la thamani kubwa.
|
5 | Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
|
6 | Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Tazama! Naweka huko sioni jiwe kuu la msingi, jiwe la thamani kubwa nililoliteua. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa."
|
7 | Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, "Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi."
|
8 | Tena Maandiko yasema: "Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu." Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo.
|
9 | Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.
|
10 | Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea.
|
11 | Wapenzi wangu, nawasihi ninyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho.
|
12 | Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu Siku ya kuja kwake.
|
13 | Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu,
|
14 | utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema.
|
15 | Maana Mungu anataka mweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya.
|
16 | Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu.
|
17 | Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waumini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme.
|
18 | Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza.
|
19 | Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili.
|
20 | Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo.
|
21 | Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili muufuate mwenendo wake.
|
22 | Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake.
|
23 | Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki.
|
24 | Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa.
|
25 | Ninyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu.
|